Jumanne, 22 Machi 2016

MABASI YA MWENDOKASI KUANZA KAZI WIKI HII

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mabasi yaendayo kasi (DART) yataanza kufanyiwa majaribio ndani wiki moja kuanzia sasa ili madereva waanze kuzoea njia na taa za kuongozea magari.
“Wataanza na mabasi kati ya 30 – 50 ambayo yatapita kwenye njia zote za mradi huo. Zoezi hilo litafanyika ili watumiaji wengine wakiwemo waendesha daladala, bodaboda na watembea kwa miguu waweze kutambua kuwa njia ya mabasi yaendayo kasi si ya kwao, hivyo waanze kuzoea,” alisema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Machi 22, 2016) wakati alipofanya ziara ya ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri iliyokuwa na lengo la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo na kukagua ujenzi wa ukuta unaotenganisha soko hilo na mabasi yaendayo kasi.
Waziri Mkuu ambaye ametembelea soko hilo kuanzia saa 5:10 hadi saa 5:54, alitoa jibu hilo wakati
akijibu maombi ya mfanyabiashara mmoja, Bw. Sharifu Ramadhani ambaye alisema wanatumia fedha nyingi kwa ajili ya usafiri kwa vile mabasi mengi yanaishia Mnazi Mmoja. “Mabasi yanaishia Mnazi Mmoja na huku ni mbali kwa hiyo tunalazimika kutembea kwa miguu kwa sababu kukodi taxi ni gharama kubwa,” alisema. Akifafanua kuhusu hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu alisema: “Hivi sasa wanakamilisha ufungaji wa mitambo ya kukatia tiketi ambapo abiria atakuwa na kadi kama za benki ambayo anaijaza fedha halafu anapita kwenye mashine, kiasi cha nauli kinakatwa halafu anaingia kwenye basi, hakutakuwa na muda wa kukata tiketi.” Alisema tatizo la usafiri kwa wafanyabiasha wa feri litakwisha hivi karibuni baada ya mabasi hayo kuanza.

DAR ES SALAAM YAPATA MEYA MPYA

Uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es Salaam ulichukua headlines siku zilizopita baada ya wananchi kuwa na hamu ya kumfahamu meya mapema, sasa leo march 22, 2016 hatimaye Diwani Isaya Mwita kupitia vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) ameibuka kidedea kwenye uchaguzi huo baada ya kuishinda CCM iliyopata kura 67, huku UKAWA wakipata kura 84, ambapo kura 7ziliharibika.

Alhamisi, 17 Machi 2016

ALICHOKISEMA MKUU WA MKOA WA MBEYA

MKUU wa mkoa waMbeya, Amos Makala, amekabidhiwa rasmi ofisi yake leo na aliyekuwa Mkuu wa mkoa huo Abbas Kandoro, huku akitoa maagizo manne mazito kwa watumishi wa serikali .Makala alisema kuwa, wakuu wote wa wilaya na wakuu wa idara katika Halmashauri za wilaya zilizopo mkoa wa Mbeya, kila siku ya Alhamisi kuanzia saa nne mpaka saa nane mchana ni marufuku kukaa ofisini bali wanatakiwa kwenda kupokea kero za wananchi vijijini nakuzishughulikia. “Mimi sijaja kutengua torati bali kutimiliza. Kila mmoja wetu atimize wajibu wake na kuacha vyeo vya uadmin wa magroup kwenye Whats App na facebook” alisema Makala.
Alisema agizo lingine hataki kusikia masuala ya ugonjwa wa kipindupindu katika Halmashauri za mkoawa Mbeya, huku akiagiza kuwa lazima mazingira yawekwe safi.

Kuhusu watumishi hewa wanaolipwa mishahara alisema jambo hilo halihitaji digrii ili kuelewa na
kulitekeleza ndani ya siku 15 kama lilivyo agizo la Rais Dkt. John Magufuli, hivyo Wakurugenzi na
maafisa utumishi wameagizwa kuwabaini haraka. “Nimekabidhiwa taarifa hapa na Mkuu wa mkoamstaafu kaka yangu Abbas Kandoro, najua kuna taarifa za upungufu wa madawati katika wilaya zetu, hivyo basi kila Mkurugenzi wa wilaya akaandike barua kuthibitisha alichopeleka kwenye taarifa yake na wala msidanganye na kuogopa kueleza ukweli ili wakati wanataka kunishughulikia mimi barua zenu ziwe ushahidi kuwa mlidanganya” alisema Mkuu huyo wa mkoa.
Aliwaeleza kuwa yeye kwa umri wake siyo mtu wa kukaa ofisini na kauli mbiu yake ni kwamba walipo wananchi, palipo na kero naye yupo na kwa sasa chini ya serikali ya awamu ya tano wanacheza mchezo uitwao usiniguse.

Jumatatu, 14 Machi 2016

WAKUU WAPYA WA MIKOA WATAAPISHWA KESHO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli amefanya uteuzi wa
wakuu wa mikoa 26 ya Tanzania
Bara ambapo kati yao 13 ni
wapya , 7 wamebakizwa katika
vituo vyao vya kazi, 5
wamehamishwa vituo vya kazi na
1 amepangiwa Mkoa Mpya wa
Songwe.
Uteuzi huo umetangazwa na
Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi
Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe
leo tarehe 13 March, 2016 Ikulu
Jijini Dar es salaam, wakuu wa
Mikoa walioteuliwa ni kama
ifuatavyo
1. Paul Makonda – Mkuu
wa Mkoa wa Dar es
salaam.
2. Meja Jenerali Mstaafu
Ezekiel Elias Kyunga –
Mkuu wa Mkoa wa Geita.
3. Meja Jenerali Mstaafu
Salum Mustafa Kijuu –
Mkuu wa Mkoa wa
Kagera.
4. Meja Jenerali Mstaafu
Raphael Muhuga – Mkuu
wa Mkoa wa Katavi.
5. Brigedia Jeneral Mstaafu
Emmanuel Maganga –
Mkuu wa Mkoa wa
Kigoma.
6. Godfrey Zambi – Mkuu
wa Mkoa wa Lindi.
7. Steven Kebwe – Mkuu wa
Mkoa wa Morogoro.
8. Kamishna Mstaafu wa
Polisi Zelote Steven –
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
9. Anna Malecela Kilango –
Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga.
10. Mhandisi Methew
Mtigumwe – Mkuu wa
Mkoa wa Singida.
11. Antony Mataka – Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu.
12. Aggrey Mwanri – Mkuu
wa Mkoa wa Tabora.
13. Martine Shigela – Mkuu
wa Mkoa wa Tanga.
14. Jordan Mungire
Rugimbana – Mkuu wa
Mkoa Dodoma.
15. Said Meck Sadick – Mkuu
wa Mkoa Kilimanjaro.
16. Magesa Mulongo – Mkuu
wa Mkoa Mara.
17. Amos Gabriel Makalla –
Mkuu wa Mkoa Mbeya.
18. John Vianey Mongella –
Mkuu wa Mkoa Mwanza.
19. Daudi Felix Ntibenda –
Mkuu wa Mkoa wa
Arusha.
20. Amina Juma Masenza –
Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
21. Joel Nkaya Bendera –
Mkuu wa Mkoa wa
Manyara.
22. Halima Omary Dendegu
– Mkuu wa Mkoa wa
Mtwara.
23. Rehema Nchimbi – Mkuu
wa Mkoa wa Njombe.
24. Mhandisi Evarist Ndikilo
– Mkuu wa Mkoa wa
Pwani.
25. Said Thabit Mwambungu
– Mkuu wa Mkoa Ruvuma.
26. Luteni Mstaafu Chiku
Galawa – Mkuu wa Mkoa
wa Songwe (Mkoa mpya).
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi
wa Mawasiliano IKULU Gerson
Msigwa, wakuu wote wa mikoa
walioteuliwa wataapishwa
Jumanne tarehe 15 March 2016
saa 3:30 Asubuhi Ikulu, Dar es
salaam.